FRUITS/MATUNDA

Kama kuna jambo ambalo si geni basi matunda ni miongoni mwao, kwani ni chakula ambacho hupatikana sehemu zote ambazo miale ya jua hutua. Matunda hutofautiana kutoka sehemu moja na nyingine kuzingatia hali ya hewa inayoruhusu ustawi wa tunda husika, mfano wenzetu wa Dodoma hufurahia zabibu, Tanga hufurahia embe, peasi na kwingineko ulimwenguni hufurahia matunda yao. 

Tunda ni nini?

Kwa lugha ya mimea tunda ni ovari iliyopea (kwa lugha rahisi iliyokomaa) na sehemu zake ikiwemo ganda na mbegu, ingawa mara nyingi tunaposikia tunda tunafikiri ni yale malaini na matamu. Tunda huweza kuwa limekauka ama kuwa na majimaji. mfano kama vile matango, nazi, machungwa, maharage pamoja na ganda lake, ndizi, njugu/karanga ndani ya ganda lake na mengine mengi tunayoyaona katika maisha ya kila siku. (Tukumbuke kuwa ovari ni sehemu ya kike ya ua).

Je, mimea yote hutoa matunda?

Si mimea yote huzaa matunda bali kundi moja la mimea ndio lina uwezo wa kutoa matunda, na hili huitwa "mimea inayotoa maua kwa lugha iliyopanda ndege (flowering plants/angiosperms). Kundi hili ndio lenye uwezo wa kutoa maua kisha yakapevuka na kupata matunda.

Matunda ni miongoni mwa vyakula muhimu ambavyo mwili unatakiwa kupata walau kwa siku mara moja. Matunda husifika kwa kuusaidia mwili kupata maji,sukari, vitamini pamoja na juzi (fibers). Ni matunda pia ambayo huupatia mwili (antioxidant) kama vile flavanoid. Ikiwa utajenga mazoea ya kula mlo wenye matunda mengi basi utajiepusha na matatizo ya moyo, kansa na kuimarisha kinga ya mwili na afya ya macho na ngozi. 

Watalam wa masuala ya lishe wameyasifia matunda na mboga kama ni vyanzo vizuri vya virutubisho na kuwa na nishati ndogo.

Faida za kula matunda 

  • Huukinga mwili kupata kansa; matunda yana antioxidant ambazo husaidia kuondoa kemikali (free radical) mwilini ambazo zikiachwa zinaweza kuudhuru mwili na kusababisha maradhi kama vile kansa.
  • Matunda ni vyanzo vizuri vya vitamini kama vile vitamini C ambayo ni muhimu kudhibiti maradhi, vitamin E ambayo husaidia afya ya ngozi.
  • Matunda ni vyanzo vya madini kama vile kalisiamu (Ca), magnesiamu (Mg), potasiamu (K) ambayo ni muhimu katika uimarishaji wa mifumo mbalimbali ya mwili ikiwemo mfumo wa fahamu, mifupa na usafirishwaji wa vitu mwilini.
  • Matunda mengi yana maji na nyuzinyuzi (fiber) , ambazo husaidia umeng'enywaji mzuri wa chakula na kuondosha tatizo la ukosefu wa choo (constipation).
  • Matunda ya machungwa,limao na ndimu, husifika kwa kuwa na vitamin C kwa wingi, antioxidants kama vile flavanoids na kuyafanya yawe muhimu katika kupambana na kudhibiti maradhi pamoja na kuimarisha kinga ya mwili.
  • Kwa akina mama wajawazito ni muhimu kula matunda kwa afya zao na ukuaji bora wa mtoto, kwani matunda yanavirutubisho muhimu, ikiwemo madini chuma ambayo yanahitajika kwa mama na mtoto.
  • Heshima ya nyumba, matunda jamii ya matango, matikiti hutajwa kuwa na kiwango kikubwa cha amino asidi ijulikanayo kama citrulline ambayo ni muhimu kwa mzunguko wa damu, hivyo husaidia katika kuimarisha nguvu za kiume.
Ushauri

  • Kwa baadhi ya watu wanaosumbuliwa na matatizo kama vile sukari ni muhimu kupata maelekezo ya daktari kuhusu matunda sahihi kulingana na afya yako. Ila wewe ambaye afya iko imara usisubiri ushauri kula iwezekanavyo.
  • Ni kawaida baadhi ya watu kutopenda baadhi ya matunda jitahidi hayo unayoyapenda ule kwelikweli.

ITOSHE KUSEMA KWAMBA "KULA MATUNDA YA KUTOSHA NI NJIA BORA YA KUIMARISHA AFYA YOTE YA MWILI NA KUJIKINGA NA MARADHI."

 Imeandikwa na Mwl.Hamadi Hamisi (BSE)

Mawasiliano: +255 743 712 150

Baruapepe: hamadihamisi395@gmail.com

Comments

Popular posts from this blog

VYAKULA VYA WANGA (CARBOHYDRATES)

MBOGA /VEGETABLES

PROTINI (PROTEIN)